Hebrews 6

1Kwa hiyo, tukiacha tulichojifunza kwanza kuhusu ujumbe wa Kristo, twapaswa kuwa na juhudi kuelekea kwenye ukomavu, tusiweke tena misingi ya toba kutoka katika kazi zisizo na uhai na imani katika Mungu, 2wala misingi ya mafundisho ya ubatizo, na kuwawekea mikono, ufufuo wa wafu, na hukumu ya milele. 3Na tutafanya hivi ikiwa Mungu ataruhusu.

4Kwa kuwa haiwezekani kwa wale ambao waliipata nuru awali, ambao walionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa kuwa washirika wa Roho Mtakatifu, 5na ambao walionja uzuri wa neno la Mungu na kwa nguvu za wakati ujao, 6na kisha wakaanguka - haiwezekani kuwarejesha tena katika toba. Hii ni kwa sababu wamemsulubisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, wakimfanya kuwa chombo cha dhihaka hadharani.

7Kwa kuwa ardhi iliyopokea mvua inyeshayo mara kwa mara juu yake, na ikatoa mazao muhimu kwa hao waliofanya kazi katika ardhi, hupokea baraka kutoka kwa Mungu. 8Lakini ikiwa huzaa miiba na magugu, haina tena thamani na ipo katika hatari ya kulaaniwa. Mwisho wake ni kuteketezwa.

9Ijapokuwa tunazungumza hivi, rafiki wapenzi, tunashawishiwa na mambo mazuri yawahusuyo ninyi na mambo yahusuyo wokovu. 10Kwa kuwa Mungu si dhalimu hata asahau kazi yenu na kwa upendo mliouonesha kwa ajili ya jina lake, katika hili mliwatumikia waamini na bado mngali mnawatumikia.

11Na tunatamani sana kwamba kila mmoja wenu aweze kuonesha bidii ile ile mpaka mwisho kwa uhakika wa ujasiri. 12Hatutaki muwe wavivu, lakini muwe wafuasi wa wale warithio ahadi kwa sababu ya imani na uvumilivu.

13Kwa maana Mungu alipompa Abrahamu ahadi, aliapa kwa nafsi yake, kwa kuwa asingeliapa kwa mwingine yeyote aliye mkubwa kuliko yeye. 14Alisema, “Hakika nitakubariki, na nitauongeza uzao wako zaidi.” 15Kwa njia hii, Abrahamu alipokea kile alichoahidiwa baada ya kusubiria kwa uvumilivu.

16Maana wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuliko wao, na kwao ukomo wa mashindano yote ni kiapo kwa kuyathibitisha. 17Wakati Mungu alipoamua kuonesha kwa uwazi zaidi kwa warithi wa ahadi kusudi lake zuri lisilobadilika, alilithibitisha kwa kiapo. 18Alifanya hivyo ili kwa vitu viwili visivyoweza kubadilika, ambavyo katika hivyo Mungu hawezi kusema uongo, sisi tulioikimbilia hifadhi tupate kutiwa moyo kushikilia kwa nguvu tumaini lililowekwa mbele yetu.

19Tunao ujasiri huu kama nanga imara na ya kutegemea ya roho zetu, ujasiri ambao unaingia sehemu ya ndani nyuma ya pazia. Yesu aliingia sehemu ile kama mtangulizi wetu, akisha kufanyika kuhani mkuu hata milele baada ya utaratibu wa Melkizedeki.

20

Copyright information for SwaULB